Wednesday, June 8, 2011

Uhuru wa vyombo vya habari, bila habari

Na Samson Kamalamo

KILA Mei 3 ya kila mwaka, ulimwengu huwa unaadhimisha Siku ya Uhuru wa vyombo vya habari duniani.

Mwaka huu kaulimbiu ya siku hiyo inasema: “Ukimya unaua demokrasia, lakini vyombo huru vya habari vinazungumza”.

Kimsingi ni kaulimbiu inayojaribu kuchochea vyombo vya habari kuzungumza zaidi na hasa masuala ya kijamii ambayo kwayo yameonekana kusahaulika.

Soma magazeti ya kila siku na kila wiki, sikiliza redio na kama haitoshi angalia matangazo ya vituo mbalimbali vya televisheni; vyote vimesheheni masuala ya siasa, mapigano na mauaji. Hivi ni kweli vyombo vya habari vipo katika kuangazia maeneo hayo tu?

Ni wazi kuna mahala vyombo vya habari vimepoteza mwelekeo na kujikuta vikishindwa kutimiza wajibu wake wa kuwapasha habari wananchi hasa zile zinazowahusu. Sitaki kuamini kuwa wasomaji wa magazeti na wasikilizaji wa redio wanavutiwa zaidi mambo ambayo yamekuwa yakiripotiwa na vyombo hivyo.

Ukweli ni kwamba hawapendi. Sisi wanahabari na mabwana zetu yaani wamiliki, ndiyo tunaoamua kipi tuwalishe wasomaji na wasikilizaji wetu. Hakika hatuwatendei haki hata kidogo.

Kwa upande wa Tanzania Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari uadhimishwa kwa namna nyingi, mojawapo ikiwa ya kuwatunikia Tuzo waandishi walioshinda katika nyanja mbalimbali za uandishi wa habari kwa mwaka mzima.

Hii inawezekana kuwa njia sahihi ya kuenzi siku hii, lakini pia bado kuna mapungufu makubwa katika tasnia hiyo ya habari nchini, kiasi cha Fikra Pevu kusema kuwa ni Siku ya uhuru wa vyombo vya habari, bila habari.

Fikra Pevu inaona ni siku ya uhuru wa vyombo vya habari, bila habari kutokana na ukweli kwamba, ziko habari nyingi ambazo zingepaswa kuandikwa, lakini haziandikwi, na kwamba waandishi wa habari wa Tanzania tunayo fursa ya kuandika mambo mengi ya msingi kuhusu nchi yetu lakini hatuandiki.

Huu ni uzembe unaostahili kupigiwa kelele na kila mwanataaluma na hata hao wanaodhamini mashindano ya wanahabari katika kuadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari.

Ingependeza kama kila mwaka kungewekwa agenda za msingi ambazo vyombo vyetu vya habari vingepaswa kuzijadili na kuzizungumzia kwa kina, halafu siku ya uhuru wa vyombo vya habari itumike kama sehemu ya kutathmini mafanikio yaliyofikiwa na hata kushindwa kufanikiwa.

Kwa mfano, ukifuatilia kwa ukaribu vyombo vyote vya habari vya Tanzania kwa miaka takriban mitatu mfululizo, vimekuwa vikiandika na kuripoti kuhusu ufisadi, si kwa kufanya uchunguzi, bali kwa kunukuu wanasiasa wakisema.

Hivi kama kweli ufisadi ni tatizo na watanzania wamechoshwa nao, jitihada gani za makusudi zimefanywa na vyombo vyetu vya habari katika kuhakikisha wanaotuhumiwa kwa ufisadi wanafikishwa katika vyombo vya sheria?

Hapa kuna mchezo wa kupoteza muda na kubadilisha mwelekeo wa fikra za watanzania, kuacha kufikiria mambo ya msingi na kuimbishwa ufisadi kila kukicha.

Kama kweli hatutumiki, basi leo hii mahakama zetu zingekuwa zimesheheni makumi kama si mamia ya kesi za ufisadi. Lakini hilo haliwezekani kwa kuwa vyombo vingine vimekuwa haviandiki habari za kina, zenye ukweli na takwimu za uhakika na za kutosha kushawishi mamlaka husika kuchukua hatua stahiki.

Nadhani ufike wakati sasa, tuachane na kushabikia hoja zinazotolewa na vyama vya siasa zenye lengo la kucheza na akili za watanzania; na vyombo vyetu viandike na kujadili masuala ya msingi.

Kwa kuwa hakuna chama hata kimoja kilichoeleza namna ya kutibu ufisadi, basi agenda za vyombo vya habari nchini zingepaswa kuangazia bei za vyakula, bei za mafuta ya petroli na namna ya kujikwamua na suala zima la mfumuko wa bei. Hayo ndiyo mambo ya msingi kwa watanzania, mambo ambayo hata siku moja hayahubiriwi na vyama tunavyovishabikia.

Siku ya uhuru wa vyombo vya habari kwa Tanzania ingepaswa kuadhimishwa kwa vyombo vya habari kutoa ushuhuda, ni kwa jinsi gani vimeweza kubadili maisha ya watanzania kwa mwaka uliotangualia na vitakavyoendelea kuboresha katika mwaka unaokuja na si kushabikia mitazamo ya kisiasa kama ilivyo sasa.

Wasalaam…

Bajeti itoe unafuu kwa maisha

Na Samson Kamalamo

VIKAO vya Kamati mbalimbali za Bunge vimekuwa vikifanyika katika Ofisi Ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam kwa takriban wiki mbili mfululizo zilizopita.

Kamati hizo, kw akiasi kikubwa zimekuwa zikipitia mapendekezo mbalimbali ya bajeti ya mwaka 2011/20112 pia kupitia ripoti kadhaa za fedha za mashirika ya umma pamoja na halmashauri.

Pasi na shaka, Kamati za Bunge zinazihusika na masuala ya fedha, zimeweza kupitia kwa makini mapendekezo ya bajeti kwa wizara mbalimbali, hivyo jukumu kubwa lililobaki ni kwa Waziri wa Fedha kuwasilisha mapendezo ya jumla bungeni, ili wabunge waanze kujadili.

Ni matumaini ya Fikra Pevu kwamba, bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012 itaangazia zaidi katika kutoa unafuu wa maisha kwa watanzania, ikizingatiwa kuwepo kwa dalili mablimbali za hali ya maisha kuendelea kuwa mbaya hata katika mwaka ujao wa fedha.

Ugumu huo wa maisha unaweza kupimwa kirahisi kwa kuangazi kupanda kwa bei ya mafuta ya petrol kila siku nchini. Ninapoandika waraka huu, tayari katika vile vituo tunavyoweza kusema kwamba vimekuwa vikiwajali zaidi wananchi, bei ya mafuta ya petrol imepanda na kufikia sh 2040/- kwa lita ukiachilia mbali wale wanaouza lita hiyo kwa sh 2070/-.

Kwa wataalamu wa masuala ya uchumi, kupanda kwa bei ya mafuta kwa namna yoyote ile, huwa kunaathiri bei ya bidhaa na huduma nyinginezo muhimu kwa maisha ya binadamu.

Hivyo basi, bei ya mafuta ya petrol inapokuwa juu, ni dhahiri bei ya beidha na huduma mbalimbali nazo huwa zinapanda na kusababisha ugumu wa maisha, kwavile uwezo wa wananchi wa kununua bidhaa kulingana na vipato walivyonavyo pia upungua.

Ni kwa kutambua namna Serikali ya Tanzania ilivyo makini katika kuwajali wananchi wake, tunaamini, kupitia bajeti ya mwaka huu, itakajribu kadri inavyowezekana kuhakikisha kunakuwepo kwa unafuu katika maisha ya watanzania.

Mathalani, kwakuwa moja ya hoja za bei ya mafuta kuwa juu ni kutokana na Serikali kwa kushirikiana na EWURA kuchukua kodi ya takriban sh 600 kwa kila lita, inaweza kupunguza viwango hivyo, na kuwezesha bei ya mafuta kushuka katika soko la ndani.

Lakini pia kwa kuwa bei ya mafuta yanayouzwa nchini huwa inapanda kutokana na muda mwingi unaotumiwa na meli hadi kupakua bandarini, basi kipaumbele cha upakuaji mizigo ungewekwa kwa meli hizo za mafuta, ili zisitumie muda mrefu. Hivyo kupunguza mzigo wanaobebeshwa watanzania na wafanya biashara wa mafuta.

Na zaidi ya hayo, tuamua kuwa mwaka huu wa fedha, ule mpango wa kuagiza mafuta kwa pamoja lazima utekelezwa, ili tuweze kuondokana na sababu za kupanda kwa bei ya mafuta zisizokuwa na msingi.

Naamini, tukisimamia katika eneo hilo la mafuta na kuhakikisha bei yake inashuka, mwaka wa fedha 2011/2012 kwa watanzania utakuwa wa neema, kwavile mfumuko wa bei uaonachangiwa na kupanda kwa bei ya mafuta, utakuwa umedhibitiwa. Zaidi tutabakia kutafuta namna ya kuondokana na vyanzo vingine vya kupandisha mfumuko wa bei.

Fikra Pevu, itaipongeza zaidi serikali endapo bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012 itawawezesha wananchi kuweza kujiweka akiba japo kidogo. Wananchi wakiweza kijiwekea akiba, utakuwa mwanzo wa uchumi kuanza kukua. Wasipoweza kujiwekea akiba, ni wazi kuwa hali yao kiuchumi itakuwa mbaya.

Tunaitakia kila la kheri bajeti ya mwaka 2011/2012 tukiamini kuwa itakuwa ya wananchi zaidi kuliko ya kuwanufaisha wafanyabiashara kama ilivyokuwa ya mwaka 2010/2011.


Serikali iko wapi?

Na Samson Kamalamo

JUMA lililopita, gazeti moja la kila siku, liliripoti kuhusu kukamatwa kwa raia wa Marekani, huko Tarime katika eneo la Nyamongo au North Mara.

Gazeti hilo liliendelea kubainisha kuwa Mmarekani huyo alikamatwa akipiga picha za matukio ya mgodi huo na kuzituma kwenda nchini kwao, haijulikani kwa matumizi gani.

Haikuelezwa kama Mmarekani huyo alikuwana kibali kutoka Idara ya Habari (MAELEZO) kumwezesha kupiga picha katika maeneo mbalimbali ya nchi tena akiwa pekee yake na kuzituma popote anapopenda.

Ninachofahamu, ni kwamba, wote wanaokuja nchi hii wakiwa waandishi wa habari au watu wengine lakini wakiwa na dhamira ya kupiga picha, wanapaswa kuwa na vibali maalum vya maeneo husika, na mara nyingi huambatana na maofisa husika, ili kuhakikisha picha zinazopigwa ni zile tu zilizoombewa kibali.

Katika hili, FIKRA PEVU haina budi kuuliza, Serikali iko wapi? Serikali inayozungumziwa hap si lazima iwe ile kuu, isipokuwa hata zile za vijiji. Ziko wapi, kiasi cha kuruhusu mgeni kufanya anachotaka katika ardhi ya nchi huru kama Tanzania?

Kitendo cha Mmarekani yule kukamatwa akifanya shughuli zake hizo hata kama ni kwa kofia ya kikundi au chama fulani, ni cha kihaini na hakipaswi kuvumbiwa macho na kuachiwa kimalizike hivi hivi tu.

Huu sasa ndiyo wakati wa kuonyesha hao wenye vikundi na washirika wawageni hao kwamba Serikali iko makini na kwamba itasimamia katika sheria na kanuni zilizopo.

Hakuna njia mbadala ya kuonyesha makucha hayo ya serikali isipokuwa kwa Mmarekani huyo na washirika wake wazalendo, wote kwa pamoja kufunguliwa mashitaka ya uhaini na kufikishwa mahakamani mapema iwezekanavyo.

Sidhani kama iko haja ya kuchelewesha jambo hilo, eti kwa visingizio vya kusubiri kukamilika kwa upepelezi. Ni upelelezi gani utatakiwa kufanyika ilhali mtuhumiwa kakutwa na ngozi?

Ngozi yake ni kamera na vifaa vingine vya mawasiliano alivyokutwa navyo eneo la tukio, vinavyomwezesha kuwasiliana na mahali popote pale ulimwenguni.

Mmarekani huyo na wengine wote walioshirikiana naye kwa misingi kwamba wanaweza kufanya lolote bila kufanywa chochote, lazima achukuliwe hatua za kisheria, hili iwe fundisho kwa wengine wanaodhani serikali imelala.

Tujiulize, ni wageni wangapi wamekuwa wakitumiwa na vikundi hivi kuchafua taswira ya Tanzania katika anga za kimataifa? Bila shaka wapo wengi, lakini kwa huyu, arobani yake imefika.

Kukakatwa kwa huyo Mmareni kunapaswa kutumiwa kama taarifa muhimu katika kubaini kwamba nchi yetu imekuwa ikiingiliwa na kuchafuliwa na watu wengi pasipo watanzania wenyewe kujua.

Hii ni dhahiri kwamba vikundi, mashirika yasiyo ya kiserikali, makampuni na hata vyama vya siasa, ama kwa kujua au kutokujua, vimekuwa vikiwezesha Tanzania kuzungumzwa vibaya huko nje na kuonekana kuwa ni taifa lisilostahili kuwepo.

Kuendelea kuvumilia vitendo vya namna hii pasipo kuvichukulia hatua kali ni sawa na kuwasaliti watanzania. Tufike mahali basi, siasa ikae pembeni na sheria ichukue mkondo wake.

Tukiendelea kuikumbatia siasa na kudhani kuruhusu kuwepo kwa maandamano kila kukicha kuwa ndiyo kuimarisha na kukuza demokrasi, huk ni kujidanganya. Ukweli tunajichimbia kaburi letu wenyewe.

Tufike mahali tupime. Na tufike mahali kubainishe wazi upi wakati wa siasa za nje yaani za majukwani na upi wakati wa siasa za ndani. Mbona huko demokrasia ilikopea hatuoni haya yanayotokea kwetu?

Fikra Pevu inaisii serikali iliyoko madarakani kuongeza uamkini kidogo na kusimamia katika sheria, hata kama kwa kufanya hivyo itaonekana kuwa inaminya demokrasia. Hiki kinachotokea sidhani kama ni demokrasia. Ni demokrasia ya wapi inayoruhusu mtu kugusa pua ya mwenzie?

Tuonane wiki ijayo. Wasalaa.

yl� o t H3 ��� 0pt;font-family:"Times New Roman","serif"'>

Hii ni dhahiri kwamba vikundi, mashirika yasiyo ya kiserikali, makampuni na hata vyama vya siasa, ama kwa kujua au kutokujua, vimekuwa vikiwezesha Tanzania kuzungumzwa vibaya huko nje na kuonekana kuwa ni taifa lisilostahili kuwepo.

Kuendelea kuvumilia vitendo vya namna hii pasipo kuvichukulia hatua kali ni sawa na kuwasaliti watanzania. Tufike mahali basi, siasa ikae pembeni na sheria ichukue mkondo wake.

Tukiendelea kuikumbatia siasa na kudhani kuruhusu kuwepo kwa maandamano kila kukicha kuwa ndiyo kuimarisha na kukuza demokrasi, huk ni kujidanganya. Ukweli tunajichimbia kaburi letu wenyewe.

Tufike mahali tupime. Na tufike mahali kubainishe wazi upi wakati wa siasa za nje yaani za majukwani na upi wakati wa siasa za ndani. Mbona huko demokrasia ilikopea hatuoni haya yanayotokea kwetu?

Fikra Pevu inaisii serikali iliyoko madarakani kuongeza uamkini kidogo na kusimamia katika sheria, hata kama kwa kufanya hivyo itaonekana kuwa inaminya demokrasia. Hiki kinachotokea sidhani kama ni demokrasia. Ni demokrasia ya wapi inayoruhusu mtu kugusa pua ya mwenzie?