Na Samson Kamalamo
VIKAO vya Kamati mbalimbali za Bunge vimekuwa vikifanyika katika Ofisi Ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam kwa takriban wiki mbili mfululizo zilizopita.
Kamati hizo, kw akiasi kikubwa zimekuwa zikipitia mapendekezo mbalimbali ya bajeti ya mwaka 2011/20112 pia kupitia ripoti kadhaa za fedha za mashirika ya umma pamoja na halmashauri.
Pasi na shaka, Kamati za Bunge zinazihusika na masuala ya fedha, zimeweza kupitia kwa makini mapendekezo ya bajeti kwa wizara mbalimbali, hivyo jukumu kubwa lililobaki ni kwa Waziri wa Fedha kuwasilisha mapendezo ya jumla bungeni, ili wabunge waanze kujadili.
Ni matumaini ya Fikra Pevu kwamba, bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012 itaangazia zaidi katika kutoa unafuu wa maisha kwa watanzania, ikizingatiwa kuwepo kwa dalili mablimbali za hali ya maisha kuendelea kuwa mbaya hata katika mwaka ujao wa fedha.
Ugumu huo wa maisha unaweza kupimwa kirahisi kwa kuangazi kupanda kwa bei ya mafuta ya petrol kila siku nchini. Ninapoandika waraka huu, tayari katika vile vituo tunavyoweza kusema kwamba vimekuwa vikiwajali zaidi wananchi, bei ya mafuta ya petrol imepanda na kufikia sh 2040/- kwa lita ukiachilia mbali wale wanaouza lita hiyo kwa sh 2070/-.
Kwa wataalamu wa masuala ya uchumi, kupanda kwa bei ya mafuta kwa namna yoyote ile, huwa kunaathiri bei ya bidhaa na huduma nyinginezo muhimu kwa maisha ya binadamu.
Hivyo basi, bei ya mafuta ya petrol inapokuwa juu, ni dhahiri bei ya beidha na huduma mbalimbali nazo huwa zinapanda na kusababisha ugumu wa maisha, kwavile uwezo wa wananchi wa kununua bidhaa kulingana na vipato walivyonavyo pia upungua.
Ni kwa kutambua namna Serikali ya Tanzania ilivyo makini katika kuwajali wananchi wake, tunaamini, kupitia bajeti ya mwaka huu, itakajribu kadri inavyowezekana kuhakikisha kunakuwepo kwa unafuu katika maisha ya watanzania.
Mathalani, kwakuwa moja ya hoja za bei ya mafuta kuwa juu ni kutokana na Serikali kwa kushirikiana na EWURA kuchukua kodi ya takriban sh 600 kwa kila lita, inaweza kupunguza viwango hivyo, na kuwezesha bei ya mafuta kushuka katika soko la ndani.
Lakini pia kwa kuwa bei ya mafuta yanayouzwa nchini huwa inapanda kutokana na muda mwingi unaotumiwa na meli hadi kupakua bandarini, basi kipaumbele cha upakuaji mizigo ungewekwa kwa meli hizo za mafuta, ili zisitumie muda mrefu. Hivyo kupunguza mzigo wanaobebeshwa watanzania na wafanya biashara wa mafuta.
Na zaidi ya hayo, tuamua kuwa mwaka huu wa fedha, ule mpango wa kuagiza mafuta kwa pamoja lazima utekelezwa, ili tuweze kuondokana na sababu za kupanda kwa bei ya mafuta zisizokuwa na msingi.
Naamini, tukisimamia katika eneo hilo la mafuta na kuhakikisha bei yake inashuka, mwaka wa fedha 2011/2012 kwa watanzania utakuwa wa neema, kwavile mfumuko wa bei uaonachangiwa na kupanda kwa bei ya mafuta, utakuwa umedhibitiwa. Zaidi tutabakia kutafuta namna ya kuondokana na vyanzo vingine vya kupandisha mfumuko wa bei.
Fikra Pevu, itaipongeza zaidi serikali endapo bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012 itawawezesha wananchi kuweza kujiweka akiba japo kidogo. Wananchi wakiweza kijiwekea akiba, utakuwa mwanzo wa uchumi kuanza kukua. Wasipoweza kujiwekea akiba, ni wazi kuwa hali yao kiuchumi itakuwa mbaya.
Tunaitakia kila la kheri bajeti ya mwaka 2011/2012 tukiamini kuwa itakuwa ya wananchi zaidi kuliko ya kuwanufaisha wafanyabiashara kama ilivyokuwa ya mwaka 2010/2011.
No comments:
Post a Comment