Sunday, October 24, 2010

Fainali imewadia, uamuzi wakwako

KWA takriban miezi mitatu, magazeti na vyombo vingine vya habari nchini, vimekuwa vikinadi siasa za vyama mbalimbali katika matoleo na machapisho yao.

Hicho kilikuwa kipindi cha kampeni kwa wagombea wa nafasi za urais, ubunge na udiwani, kila mmoja akijaribu kujiuza ili apate kununuliwa. Ndiyo biashara matangazo, na wagombea walikuwa na kila sababu ya kujitangaza ili kwanza wafahamike, lakini pili wakubalike na tatu wanunulike au wachagulike.

Mbinu za kila aina tumeshuhudia zikitumika katika kujinadi huko, zikiwemo safi na chafu, ili mradi mgombea atengeneze mazingira ya kuwa na mvuto kwa wapiga kura.

Wapo baadhi ya wagombea, tunawajua, walidiriki hata kudandia mambo ya uongo yaliyozushwa katika jamii, kwa lengo la kuyatumi akama silaha ya maangamizi dhidi ya viogozi wengine, lakini katika kipindi kifupi tu waliweza kuumbuka, baada ya ukweli wa mambo kuwekwa wazi.

Najua na ninatambua kuwa siku zote kama ilivyo katika vilabu vya mpira wa miguu, huwa wapo washabiki damu. Washabiki ambao huwa hawasiki la mwazini wala la mnadi sala. Wako tayari kushabikia jambo fulani hata kama halina ukweli na maslahi kwa nchi. Hawa hatuna jinsi ya kuwabadili msimamo wao na si makusudi ya safu hii kuwabadili watu hao.

Ninachotaka kusema ni kuwa, tumebakiza siku tano tu kufanya maamuzi makubwa na mazito kwa nchi yetu. Naamini kila mmoja wetu kwa njia moja ama nyingine ameshiriki katika kampeni zilizoanza Augosti 20 mwaka huu hata kama si moja kwa moja au kwa kuhudhuria mikutano ya kampeni katika viwanja mbalimbali.

Ni wazi kuwa hapo ulipo sasa tayari umekwisha kufahamu mgombea yupi unapaswa au ungependa kumchagua ili awe kiongozi wako kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Uamuzi ni wako na una kila sababu ya kuwa huru, lakini unapaswa kujiuliza mara mbili, je huyo unayetaka kumchagua ni kwa kiasi gani ataweza kutimiza ahadi alizotoa majukwaani?

Ni vema ukajiuliza katika hili, ili usije ukafanya maamuzia mbayo pengine yataturudisha nyuma kuliko hapa tulipofikia. Ukidhani kwamba mgombea kipenzi chako anaweza kuleta mabadiliko katika Kata yako, Jimbo na hata nchi basi jitokeze kupiga kura ifikapo Oktoba 31, mwaka huu.

Hapa nina maana kwamba, pamoja na uamuzi ulijikita katika kichwa chako hivi sasa, bado unayo fursa ya kutumia hizi siku tano zilizobakia kumpima mgombea udiwani, ubunge na urais ambaye ndiye chaguo lako kama anafaa. Wakati mwingine si lazima kumchagua swahiba wako kuwa kiongozi endapo uanamini au unadhani kuwa hawezi kutimiza ndoto zako.

Tunachopaswa kufahamu ni kuwa, ushabiki wa aina yoyote ile haupaswi kutawala mawazo, fikra na maamuzi yetu katika kuchagua viongozi. Nafikiri tunapaswa kuwa makini zaidi katika kipindi hiki kuliko wakati mwingine wowote, kwakuwa kosa tutakalolifanya litatugharimu kwa miaka mitano ijayo, labda tu itokeo vinginevyo.

Shime mtanzania mwenzangu usiweke nyuma na kushindwa kupiga kura Oktoba 31. Endapo utakuwa mzima wa afya, jitokeze wewe na familia yako na wote waliofikisha umri wa kupiga kura, kutumia haki yenu hiyo ya msingi, kikatiba na kidemokrasi ya kuingiza viongozi madarakani, kwa umakini mkubwa.

Nasisitiza upige kura kwa umakini kwakuwa ukishapiga kura na kwa bahati mbaya ukafanya uchaguzi batili, hautakuwa na fursa ya kufanya mabadiliko kwakuwa mfumo huo wa demokrasia haupo na haujapata kutumika katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Itakulazimu kusubiri kwa miaka mitano ndipo ujisahihishe.

Waungwana, fainali imewadia, uamuzi ni wa kwako. Jitahidi kufanya maamuzi sahihi, ili uendelee kuwa na furaha katika miaka mitano ijayo. Furaha na majuto yako mikononi mwako, huna sababu ya kujuta wakati fimbo unayo mkononi. Kila la kheri katika uchaguzi mkuu, usibaki nyumbani, jitokeze kupiga kura kumchagua yule unayeona anafaa kuwa kiongozi wa eneo lako, jimbo na hata nchi.

Wasalaam,

Tunahitaji serikali ndogo, makini

HAPANA shaka singo mpya za kampeni ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, zinaelekea ukingoni kusikika. Kwa ambao hawakupata bahati ya kurusha singo zao, wasubiri 2015.

Kumalizika kwa singo hizo, hakuashirii kitu kingine chochote, zaidi ya kupata serikali mpya, wabunge na madiwani wapya.

Kupatikana na kwa serikali mpya, yaani Rais aliyeko madarakani kuchaguliwa tena kwa kipindi cha miaka mitano au kuchaguliwa kwa Rais mpya kabisa, jambo ambalo si rahisi kutokea kwa mazingira yetu kwa sasa, kunaibua hisia na matumaini mapya ya wananchi juu ya serikali hiyo.

Ni kwa kutambua kwamba watanzania watakuwa na hisia na matumaini mapya kutoka kwa yoyote atakayeshikilia usukani huo wa urais, nimeona iko haja ya kutumia safu hii kueleza nini watanzania tunahitaji kutoka kwa Rais huyo.

Ama kwa mtazamo wa safu hii kama nilivyoeleza hapo awali, hapana shaka hata kidogo, Rais aliyeko madarakani, Jakaya Kikwete atarejea tu hata kwa ushindi mwembamba wa kura mbili dhidi ya wapinzania wake.

Ukweli hili halina ubishi, kwamba tukiangazia matokeo kura za maoni yaliyoendeshwa na mashirika mbalimbali ya utafiti nchini yakiwemo REDET na Synovate.

Kwa matokeo yale, licha ya kuwepo kwa kauli za hapa na pale za wanaojiita wanaharakati wa kutetea haki na maslahi ya watanzania, bado hakuna ubishi kati ya wagombea wanaoshindana na JK hakuna wa kumshinda.

Inaweza kusemwa kwamba nimekurupuka kuweka bayana kile ninachoamini, lakini kwa mazingira ya Tanzania na Afrika kwa ujumla, hata Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), itakubaliana nami kuwa upinzani bado hauna nafasi.

Ndiyo, historia inaonyesha kuwa upinzani ulipata kufanikiwa Kenya, Zambia na Malawi tukizungumzia mifano michache, lakini huko kwa wenzetu kuna mazingira tofauti. Kwa waliofika katika nchi hizo wanatambua na hata wapinzani wenyewe wanatambua.

Kwa Tanzania kuwa na madiliko ya Chama itatuchukua muda mrefu kutokana na sababu nyingi, mojawapo ikiwa ni ya uelewa finyu au duni wa sera na mchakato mzima wa mfumo wa siasa ya vyama vingi. Vyama vyetu kama vilivyo vyombo vyetu vya habari, bado ni vya wakazi wa mijini tu. Huu ndiyo ukweli, na kwa jinsi hii, upinzani utafanikiwa pale utakapoweza kuwafikia asilimia 50 ya watanzania.

Kwa kuwa hakuna takwimu sahihi za idadi gani ya watanzania wamefikiwa na kuelimishwa kuhusu mfumo wa siasa wa vyama vingi na umuhimu wake kwao na maendeleo yao, bado tutalazimika kukubali kuendelea kuongozwa na CCM, na kwa maana hiyo, hatuna sababu ya kukwepa adui kama anavyofanya Mbuni kwa kufukia kichwa huku kiwiliwili kiko hadharani.

Kwa vile dalili zipo kuwa JK atatuongoza kwa miaka mingine mitano na kwa kuwa yapo mengi yamesemwa mtaani kuhusu awamu ya kwanza ya serikali ya Kikwete, iko haja ya kuwepo kwa mabadiliko katika awamu ya pili ya uongozi wake.

Katika awamu hiyo, safu hii, ingemshauri JK aunde Baraza dogo la Mawaziri, makini ambalo litakuwa tayari kutekeleza maagizo atakayokuwa anatoa. Baraza hilo kuundwa na timu kubwa ya watu kutokana wabunge kumi ambao Kikatiba, JK atakuwa na haki ya kuwateua.

Safu hii inapendeza hivyo kwa kuamini kuwa, wabunge utakao wateua kutoka miongoni kwa watanzania milioni 40 wenye sifa ya kuwa viongozi, lakini kwa sababu mbalimbali wameshindwa kuingia kwenye siasa, hapa shaka watakuwa mawaziri na watendaji wazuri na hawatakuwa tayari kukuangusha kwa lolote, kwa kuwa hawatakuwa na jeuri ya kusema kuwa wamechaguliwa na wananchi.

Hata hivyo, unaweza kuteua wabunge kutoka katika majimbo kuwa mawaziri, lakini kigezo kikubwa kikiwa uadilifu wao kwako na kwa watanzania, utendaji na utayari wao wa kulitumia taifa hili kwa moyo mmoja, kama ilivyopata kuwa kwa John Magufuli wakati ule akiwa Waziri wa Ujenzi.

Hizo ndizo salamu za safu hii kwako na kukukumbusha kuwa kweli rafiki ni bora lakini si mara zote. Wakati mwingine anaweza kuwa kikwazo cha wewe kufikia mafanikio au malengo uliojiwekea.

Nawatakia maandalizi mema ya kupiga kura Oktoba 31, mwaka huu.

NEC teknolojia izae matunda mema

JUMA lililopita Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitangaza kwamba matokeo ya kura za urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu yatakuwa ya kwanza kutolewa kabla ya matokeo ya ubunge na udiwani.

Kwetu watanzania hii ni faraja kubwa ikizingatiwa kwamba katika miaka iliyopita, matokeo yalichukua siku tano hadi kumi kutokana na mfumo wa ukusanyaji taarifa za matokeo ulivyokuwa, pamoja na jiografia ya nchi yetu.

Mwaka huu NEC imeamua kutumia teknolojia ya kisasa ya mawasiliano ambapo haichukui muda mrefu kwa matokeo ya kura za aina yoyote kuweza kuwekwa bayana kwa taasisi na jamii husika.

Haya naweza kusema ni mapinduzi, kwakuwa yatatuwezesha watanzania kumfahamu kiongozi mpya wa Tanzania katika kipindi kifupi baada ya watanzania kutumia haki yao ya msingi ya kumchagua Rais wao.

Ni dhahiri kuwa wapiga kura 19,686,608 waliojiandikisha kwa ajili ya kupiga kura Oktoba 31 mwaka huu, watakuwa na fursa nzuri ya kutambua matokeo ya maamuzi yao, pasipo kuwepo kwa uwezekano wa namna yoyote ile ya matokeo hayo kuchakachuliwa.

Fikra Pevu inaipongeza NEC kwa utaratibu huo mpya, kwakuwa umekuja wakati muafaka na inaamini kuwa utaondoa fikra za kuwepo kwa mazingira ya kura za rais kuchezewa na kutolewa matokeo yasiyo haki.

Ni kwa mantiki hii, vyama vya siasa nchini vinapaswa kujiweka tayari kupokea matokeo yoyote yatakayotolewa na NEC, siku moja baada ya watanzania kupiga kura.

Hatutarajii kwa vyovyote vile baada ya matokeo hayo ya urais kutangazwa tena kwa kushirikisha mawakala wa vyama katika vituo vyote vya kupigia kura, kutajitokeza madai ya kutokukubalina na matokeo yatakayotangazwa.

Ni vema kupitia uchaguzi huu wa nne wa demokrasia ya vyama vingi, wanasiasa na hasa wagombea, wakajifunza namna ya kukubali matokeo hata kama yatakuwa kinyume cha matarajio yao.

Kukubali matokeo, ni dalili za kukomaa kisiasa na hakuna sababu kwa wanasiasa wa Tanzania kuendelea kuwa wachanga ilhali mfumo wa siasa za Tanzania unaendelea kukua na kuimarika kila siku.

Kwakuwa NEC imeamua kutumia mfumo mpya wa kuwezesha kupatikana kwa matokeo kwa muda mfupi zaidi, ni wazi kuwa mfumo huo utazaa matunda mema na utakuwa chachu ya mabadiliko na maendeleo ya kidemokrasia nchini Tanzania.

Kama ambavyo teknolojia ya mawasiliano ilivyoweza kufanya kazi vema nchini Kenya mwaka 2007, ndivyo ambavyo tunaamini itatumika kutoa matokeo mema katika uchaguzi mkuu wa Tanzania mwaka huu.

Kwa utaratibu huu, tunaamini watanzania watakuwa na fursa ya kukwenda sanjari na mabadiliko ya kiteknolojia ambayo siku zote yanaaminika kutoa matokeo sahihi endapo hapatakuwepo na wajanja wachache watakaoamua kucheza matokeo hayo kwa maslahi yao binafsi.

Fikra Pevu inaamini kuwa hapatakuwepo na uchezeaji wa namna yoyote wa matokeo ya uchaguzi wa mwaka huu, ili kupunguza uwezekano wa kuwepo au kujitokeza kwa malalamiko ya aina yoyote ile. Kama upo uwezekano wa kuepuka malalamiko, basi nguvu za ziada zitumike kuondosha malalamiko ya aina hiyo.

Rai ya safu hii ni kwamba NEC itumie hiyo teknolojia mpya katika kuharakisha kupatikana kwa matokeo, izae matunda mema na si machungu.

Tuonane Juma lijalo.

Ahadi sawa, mbichi au mbivu juu yetu

NINAPOANDIKA waraka huu, zimebaki siku 25 tu kwa watanzania kutafakari hatima ya taifa lao.

Zitakapokwisha siku hizo 25, ile ya 26 yaani Oktoba 31, itakuwa ni siku ya kufanya maamuzi mazito juu ya taifa hili linaloendelea.

Ni siku ya kila mtanzania aliyejiandikisha kupiga kura na ambaye jina lake lipo sahihi katika daftari la wapiga kura, atatumia haki yake ya kikatiba ya kumchagua yule anayedhani anafaa kuwa kiongozi wa taifa ili kwa miaka mitano ijayo.

Tunapozungumzia uchaguzi, mara nyingi tunazungumzia Rais,Wabunge na Madiwani. Lakini katika muktadha huu wa leo, nataka tu kuwakumbusha watanzania kuwa makini katika kufanya maamuzi hayo mazito.

Kimsingi ni maamuzi ambayo hayahitaji kufanyiwa majaribio, ukitaka kufanya majaribio, majuto yatakuwa haki yako, na usipojitokeza kabisa kupiga kura, hautakuwa na haki ya kuinua mdomo kulaumu maamuzi watakayokuwa wamefikia wenzako.

Pamoja na kwamba uchaguzi unahusu wagombea urais, ubunge na udiwani, mkazo mkubwa upo katika kuchagua nani awe Rais wa nchi katika kipindi cha uongozi wa miaka mitano kuanzia mwaka 2010.

Najua na ninatambua kuwa kuanzia Agosti 20 mwaka huu tumekuwa tukisikia na kuwaona wanasiasa wengi wakisimama majukwaani kunadi sera na ilani za vyama vyao. Hawakuishia hapo, wengi wao wamekwenda mbali kiasi cha kutoa ahadi kemkem.

Kweli ahadi ni sawa kabisa. Hata sisi wenyewe kwa wenyewe mara nyingine tumekuwa tupeana ahadi mbalimbali za kutiana moyo, lakini tujiulize ni mara ngapi ahadi hizo zimepata kutimizwa.

Kwa kuwa wengi wetu tupo masikini, na hatuna uwezo, tumejikuta ahadi zetu nyingi zikiyeyukia hewani kwa kukosa nyezo za kutumia katika kuzitekeleza. Zimebaki kuwa ahadi hewa.

Ni kwa kigezo hicho, ndipo napotaka kuwaasa watanzania wenzangu kuwa makini katika kutumia hiyo haki yao ya kikatiba.

Ni vema mkatumia muda huu uliobaki wa siku 25 kupima ahadi zilizotolewa na wagombea mbalimbali wa nafasi ya Urais, kupata uhakika wake wa kuweza kutimizika.

Nisingependa mzipime ahadi hizo kwa uzuri wake wa mapambo ya lugha zilizotumika, bali kwa uhalisia wake kwa kuzingatia mazingira ya Tanzania na uwezekano wa kutekelezeka kwake.

Tuwapime wagombea wetu kwa kutumia vigezo mbalimbali, ambapo yule tutakayeona anayo nafasi kubwa ya kutimiza ahadi zake, basi tumpe fursa hiyo, badala ya kuwapa wengine ambapo kwa hakika itawalazimu watumie muda mwingi kujipanga hadi waje kufikia hatua ya kuanza kutekeleza ahadi zao hizo.

Ikumbukwe kuwa katika ulimwengu wa siasa, hakuna muda wa majaribio. Muda uliopo kila siku ni wa kutenda na kutekeleza ahadi zilizopo na zinazotolewa.

Hofu yangu ni kwamba, tusije tukatumia njia ndefu kupata maji ya kukata kiu yetu, wakati maji tayari tunayo mkono. Tunachotakiwa ni kujadiliana jinsi ya kuendelea kuyanywa tena tukiwa tumejikalia kivulini.

Hivyo basi, ni juu yetu watanzania kuchagua mbichi au mbivu ifikapo tarehe 31 Oktoba, 2010. Uamuzi unao mwenyewe, usipojitokeza utakuwa ujinga wako na ukimchagua atakayekuja kukurudisha nyuma ni uzembe, kwa kuwa utakuwa umepoteza muda, ambao ni kutu cha thamani sana kuliko kingine katika maisha yako.

Siku ya siku ikifika, tujitokeze kwa wingi na tufanye maamuzi sahihi pasipo kushawishiwa au kurubuniwa wa yeyote. Zimwi likujualo halikuli likakwisha.

Chadema msivuruge uchaguzi

KATIKA moja ya habari za gazeti hili, kunazungumziwa namna Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilivyojizatiti kuhakikisha kinapata ushindi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Katika suala la uchaguzi kama ilivyo katika mpambano wa mpira wa miguu, huwa kuna kufa au kupona katika kusaka ushindi.

Zipo baadhi ya timu uenda mbali zaidi na kufikia hatua ya kutumia Kamati za Ufundi ili mradi wahakikishiwe kupata ushindi dhidi ya wapinzani wao.

Sidhani kama Kamati za Ufundi zinatumika pia katika vyama vya siasa hasa kwenye harakati za kusaka ushindi! Kama zinatumika, basi wanasiasa wetu ndiyo wenye nafasi kubwa ya kutujuza namna wanavyotumia kamati hizo kujinyakulia ushindi.

Katika siasa za kimaendeleo ambazo naamini Tanzania tunazifuata, kinachokipa chama fulani ushindi ni aina ya mgombea aliyesimamishwa, sera za chama husika na Ilani ya uchaguzi wa chama hicho.

Pale chama kinapochagua mgombea ama asiyeuzika au asiye na mvuto, ni dhahiri kuwa chaka hicho kitakuwa na asilimia kubwa ya kupoteza ushindi. Lakini pia uzoefu unaonyesha kuwa katika Tanzania yetu, bado suala la kufahamika kwa chama limekuwa mtaji mkubwa wa chama husika kupata ushindi.

Kwa mantiki hiyo ni kwamba, kama chama chako hakifahamiki, hakina mchango wowote unaonekana kwa wananchi, hata ufanye kitu gani, kamwe hautapata ushindi, utakuwa tu unauza maneno.

Ni kwa hoja hizo hapo juu, ndipo narudi kwenye mada ya leo ya rafiki zangu CHADEMA ya kutaka kuchukua hatua za kujitangazia ushindi kabla Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haijatangaza.

Ni kweli CHADEMA kama chaka kinacho kila sababu ya kujua na kufahamu idadi gani ya kura za ndiyo na hapana zimepigwa katika kituo fulani na chama gani kimepata kura nyingi, halikadhalika chama kipi kimepata kura kidogo, lakini si kujitangazia ushindi.

Rafiki zangu hawa wakifikia hatua ya kujitangazia ushindi, ni wazi watakuwa wamekiuka taratibu na kanuni za uchaguzi za nchi hii, na kwa maana nyingine wataufanya uchaguzi usiwe huru na haki.

Nisingependa CHADEMA waingie kwenye doa la kuvuruga uchaguzi na nchi kwa ujumla. Hata kama wanadhani kuwa huwa wanaibiwa kura zao, ni vema wakakusanya takwimu na kuziwasilisha zinakohusika, ikibidi kura za eneo fulani zirudiwa kuhesabiwa au uchaguzi wa jimbo husika ufanyike upya, lakini si kujitangazia ushindi.

Kama CHADEMA wataamua kujitangazia ushindi katika kila jimbo wanalodhani kuwa wataibuka na ushindi, itakuwaje CUF, CCM, TLP, NCCR-Mageuzi na vyama vingine navyo vikiamua kufanya hivyo?

Ningependa na ningeshauri rafiki zangu CHADEMA watumie busara kidogo katika kuendesha na kufanikisha uchaguzi huru na haki nchini, badala ya kuwa chanzo cha vurugu na mfarakano.

Ndiyo, wanaweza kabisa kuwa chanzo cha vurugu na mfarakano kama ilivyotokea nchi jirani ya Kenya, endapo watapinga matokeo yatakayotangazwa na NEC kwa kigezo kwamba matokeo hayo hayawiani na waliyonayo.

Ni vema CHADEMA wakasubiri matokeo ya kura zitakazopigwa Oktoba 31 mwaka huu yakatangazwa na chombo husika, badala ya wao kujivisha majukumu ya NEC na kujitangazia matokeo.

Tutakuwa na hakika gani kwamba matokeo yatakayotangazwa na CHADEMA yatakuwa ya haki ilhali naye ni mshindani katika kusaka madaraka ya kisiasa ya nchi hii?

Kama kweli wanajiamini na kujihakikishia kuibuka na ushindi, wana sababu gani ya kuharakisha kutangaza matokeo? Hapa kuna jambo na huenda si dogo kama ambavyo wengi wetu tunadhania.

Napenda kumalizia kwa kutoa rai kwa ndugu zangu wa CHADEMA pamoja na jukumu kubwa mlilonalo la kulinda kura zenu, ni vema misingi, taratibu, kanuni na maadili ya uchaguzi huru na haki ikafuatwa, ili kuepuka vurugu, ghasia na mifarakano isiyokuwa na maana.

Kushindwa leo hakuna maana ya kushindwa daima, huenda bado hujafikia kiwango cha kukubalika na kuaminika. Matokeo yoyote ya uchaguzi yanapaswa yachukuliwe kama fursa ya kufanya vema katika uchaguzi mkuu utakaofuata, ndivyo demokrasia inavyosema. Hii ni kwa vyama vyote na si kwa CHADEMA tu.

Tuwasiliane wiki ijayo.

Seif, serikali tatu!

MOJA ya mambo yanayonivutia sana katika siasa za Tanzania, ni kule kutaka kuziendesha kinyume na wenzetu wanavyo kwenda.

Inawezeka hiyo ikawa sababu ya Taifa hili kushindwa kusonga mbele na hata kurudi nyuma hadi leo. Tutasongaje mbele kama tunaweza kuwa na viongozi wanaofikiria kwenda kinyume na wenzao wanavyokwenda?

Ukisikiliza ahadi nyingi zinazotolewa majukwaani hivi sasa kama sehemu ya kuvutia wapiga kura, wanadi sera na ilani za vyama wamekuwa na ahadi kemkem.

Sikatai majukwaa hayo ya kisiasa kutumia kutoa ahadi hizo, kwa kuwa chaguzi zote zile duniani iwe Afrika, Ulaya na hata Marekani, hushehenezwa na ahadi za kila aina ili mradi kumvutia mpiga kura.

Ni kupitia ahadi hizo, ndipo wapiga kura wa Tanzania, Oktoba 31 mwaka huu, watatumia fursa yao ya kuchagua zile ahadi wanazoamini kuwa zitatekelezeka kutokana na uimara na ubora wake, na si vinginevyo.

Pamoja na kuwa ahadi ni sehemu ya kampeni, naweza kusema kwamba si kila ahadi inaweza kutekelezeka na si kila ahadi inaendana na hali halisi ya mazingira, siasa na uchumi wetu Tanzania kama taifa na maslahi ya nchi wahisani wa Tanzania, kama wadau wa demokrasia nchini.

Kweli tunatakiwa kutoa ahadi, lakini si ahadi zinazokwenda kinyume na taratibu zinazoongoza na kutawala dunia. Hatuishi katika kisiwa, hivyo hatupaswi kuwa na mitazamo na mienendo tofauti na pande nyingine za dunia.

Hata huko kwenye mataifa yaliyoendelea kama Marekani, Uingereza, Japan, Ujerumani, China, India na hata hapa katika nchi za Afrika zilizoko mbele kiuchumi kuliko sisi, huduma za afya na elimu hazitolewi bure kwa kila mmoja. Sasa hawa ndugu zetu wanaokuja na ahadi za kutoa huduma hizo bure, nguvu na ubavu wa kusema hivyo wanautoa wapi? Hapa ndipo hoja ya Mrisho Mpoto ya kumpa mbu kazi ya kutibu malaria inapokuwa na mashiko.

Kama hilo halitoshi, mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF Maalim Seif Sharif Hamad wiki iliyopita naye akaja na mpya ya kuturudisha nyuma, nayo si nyingine isipokuwa hoja ya serikali tatu.

Hivi ni kweli watanzania wanataka serikali tatu au ni mbinu ya kuwalaghai wapiga kura? Tunazungumziaje serikali tatu leo wakati dunia nzima inazungumzia kuungana? Tunapokuwa na serikali tatu tunaimarisha muungano au tunaudumaza?

Nafikiri ahadi za namna hii ni za alinacha na hazipaswi kupewa uzito hata kidogo katika jamii yenye fikra endelevu kama ya Tanzania. Ni kwa mkakati huo huo wa kudai serikali tatu, rafiki yangu Mchungaji Christopher Mtikila mara zote amejikuta akishindwa kisiasa kwa hoja yake ya serikali ya Tanganyika. Ndiyo anayohaki ya kuipigania, lakini si wakati huu.

Natambua CUF ni chama makini pengine kuliko vyama vyote vya upinzani vilivyopo, nisingependa hoja hii itumike kuwaangusha katika safari yenu ya kisiasa visiwani Zanzibar na hata Bara. Natoa rai hiyo kwa sababu natambua wenzenu wataitumia katika kuwapigilia msumari.

Katika uchaguzi huu, hoja ya serikali tatu haina mashiko hata kidogo, badili upepo Seif kabla haujakubadilikia.

Tukutane juma lijalo panapo majaliwa.

UNDP, MCT mkuwa wapi?

NIKIWA Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Klabu ya Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC), Juma lililopita nilipata fursa ya kuhudhuria mafunzo ya siku moja.

Mafunzo hayo yaliyofanyika mjini Kibaha, Pwani na kudhaminiwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), yalilenga katika kuwafundisha waandishi wa habari wa Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na Tanga mwongozo wa maadili katika kuripoti habari za uchaguzi mkuu 2010.

Mwongozo huo muhimu kwa wanahabari na vyombo vya habari hasa katika kipindi hiki cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu, unabainisha maeneo kumi na matano muhimu katika uandishi wa habari makini na unaozingatia kanuni.

Maeneo hayo ni pamoja na kutokupendelea, kuandika ukweli, kuitikia mahitaji ya wapiga kura, kuhamasisha uhuru wa maoni, kulinda vyanzo vya habari, kuepuka matamshi ya chuki na uchochezi, kukuza tunu za demokrasi na wajibu wa vyombo vya habari na wamiliki wake.

Mengine ni kufanya uchunguzi wa hoja, kuwa na bei zinazowiana za matangazo, vyombo vya habari kufanya kazi kulingana na matakwa ya sheria ya uchaguzi, vyombo vya habari kushirikiana na jumuia za kiraia, kuepuka makosa ya kitaaluma, kuwa makini na kura za maoni na vyombo vya habari kukuza ushiriki wa makundi maalum katika kupata nafasi za uongozi wa kisiasa.

Ukiangalia kwa undani vipengele hivyo vya mwongozo wa maadili katika kuripoti habari za uchaguzi mkuu 2010, unabaini kuwa vina umuhimu mkubwa sana si tu kwa vyombo vya habari na wanahabari, bali hata kwa jamii. Lakini swali la kujiuliza UNDP na Baraza la Habari Tanzania (MCT) walikuwa wapi siku zote hadi waje kutoa mafunzo leo hii wakati kampeni zimeanza? Vyombo vitayapigiaje makundi maalum wakati tayari yalishaachwa nje ya ulingo?

Wanaweza kusema kwamba walianza mapema kutoa mafunzo hayo, lakini taarifa zinaonyesha kwamba Jukwaa la Wahariri liliridhia mwongozo huo katika warsha iliyofanyika Agosti 13 mwaka huu mjini Morogoro na kwamba wadau wa habari nao waliridhia katika mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam Agosti 18 mwaka huu.

Kwa yeyote anayetambua umuhimu wa mwongozo wa maadili ya kuripoti habari za uchaguzi mkuu, anaweza kukubalina na Fikra Pevu kwamba mafunzo na kuridhiwa kwa mwongozo huo kumekuja tayari kukiwa kumekucha.

Ni kwa muktadha huo, ni vema basi taasisi zinazohusika zikafikiria namna ya kutoa mafunzo ya jinsi hiyo mapema kabla mchakato wa jambo husika haujanza, ili taasisi hizo ziwe na fursa nzuri ya kufuatilia yupi alifuata maadili na yupi alipotoka.

Huenda haya tunayoyashuhudia hivi sasa ya vyombo vya habari kugawanyika katika mchakato wa kupata viongozi wa taifa hili ni kutokana na maadili hayo kutokufahamika na waandishi pamoja na wahariri wao.

Lakini pengine kunaweza kuwa ndiyo ukomavu wa demokrasia kwa vyombo vya habari kushiriki ipasavyo kumwingiza au kumng’oa madarakani mgombea fulani.

Aina hii ya uandishi wa habari unaonekana hapa nchini hivi sasa, unaweza kuushuhudia nchini Marekani ambapo ni jambo la kawaida wakati wa uchaguzi, gazeti fulani kujiweka wazi kuwa litaendesha kampeni kuhakikisha mgombea fulani anaingia madarakani.

Hiyo huwa haijalishi kama gazeti hilo ni la chama husika ama la. Jambo kubwa linalozingatiwa na gazeti huwa ni sera za mgombea na Ilani ya uchaguzi ya chama, kwamba kikiingia madarakani, kitawafanyia kitu gani wamarekani.

Kwa mantiki hiyo, kama vyombo vya habari vya Tanzania vinadhani demokrasia imepanuka kiasi cha kutosha, ni vema vikaweka wazi upande vinaposhabikia badala ya kuyumbisha wasomaji na wananchi. Ni vema vikasema kuwa tuunga mkono ama Ari Zaidi, Nguvu Zaidi na Kasi Zaidi au Hatudanganyiki, badala ya kudemadema.

Naamini vyombo vya habari vikionyesha kule vipoangukia, itakuwa rahisi kwa UNDP na MCT mwaka 2015 kujua mwongozo wa maadili ya kuripoti habari za uchaguzi uweje, kwa kuwa tayari vyombo vitakuwa vimekwisha kujipambanua.

Bajeti poa, tuitekeleze

NINAYO kila sababu ya kumpongeza Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustapha Mkulo kwa hotuba nzuri ya bajeti aliyoitoa bungeni mjini Dodoma wiki iliyopita. Kwa hakika, hotuba hiyo inaonyesha mwanga wa mwelekeo chanya kiuchumi.

Ongezeko la bajeti hiyo kwa kiasi cha shilingi 1.6 trilioni ilinganishwa na bajeti ya mwaka wa fedha 2009/2010, si haba na wala si jambo la kubeza. Ni jambo la kuunga mkono na kutoa ushirikiano wa dhati, kuhakikisha inatekelezwa kama vile inavyopangwa.

Kusimamiwa na kutekelezwa vema kwa bajeti hiyo, hapana shaka pataiwezesha Serikali ya awamu ya nne kufikia malengo yake iliyojiwekea na hasa ya kuleta nafuu ya maisha kwa wananchi wake.

Ni kweli bajeti hiyo imezingatia mambo mengi kiasi cha kuwepo kwa ongezeko katika maeneo muhimu kwa maendeleo ya Taifa na wananchi kwa ujumla. Ukiiangalia kwa makini, utabaini kuwa katika elimu kumekuwepo na ongezeko la aslimia 17.2, miundombinu 37.7%, kilimo 35%, afya 25.2%, nishati 14.6 na maji 14.5. Hili ni ongezeko kubwa katika bajeti na endapo litatekelezwa kama vile ilivyopangwa, tutashuhudia kutokea kwa maajabu Tanzania.

Kwa mtazamo wa haraka haraka, hapana shaka yoyote kwamba bajeti hii inaweza kuleta mabadiliko makubwa katika jamii, pale tu tutakapothubutu kuhakikisha hakuna yeyote anayeweza kucheza nayo au kuzorotesha juhudi za kuitekeleza.

Fikra Pevu inatoa onyo hilo kwa kuzingatia ukweli kwamba katika miaka ya hivi karibuni, wamejitokeza watu wasioitakia mema serikali iliyopo madarakani na kuamua kuihujumu vile wanavyopenda au wanavyoona inafaa. Watu hao ambao wengine ni maofisa waandamizi, wamediriki kuzorotesha mipango na miradi yote ya maendeleo ili mradi serikali ionekane haijafanya chochote.

Kuendelea kuwaacha maofisa wa namna hiyo kuwepo katika ofisi hizo za umma, ni sawa na kuwasaliti wananchi na pia ni kusaliti juhudi zinazofanywa na maofisa wachache waaminifu wa serikali, walioko tayari kutii maagizo ya viongozi na watendaji wakuu wa serikali. Kushindwa kutekelezwa kwa bajeti mathalani hii ya 2010/11, hakutakuwa na dosari kwa maofisa wa serikali, isipokuwa itakuwa doa kwa serikali ya Rais Jakaya Kikwete. Hii yote ni kutokana na yeye kuwa kinara wa serikali hivyo kila baya kubebeshwa yeye hata kama hausiki.

Njia pekee ya kuondokana na hali hiyo, ni kuhakikisha kila ofisa wa serikali pale alipo, anatimiza wajibu wake vile inavyopasa na ndani ya muda wa kazi, yaani saa 2 asubuhi hadi 9:30 alasiri na si kufanya kazi hizo katika muda wa ziada ili kudai exta duty allowances.

Ningekuwa mimi mwamuzi, posho za muda wa ziada zingetolewa tu pale inapoonekana iko haja ya kutolewa kwake hasa kutokana na mtumishi kushindwa kumaliza majukumu yake katika muda wa kawaida, na kwamba aliutumia vema muda huo wa kawaida bila mafanikio. Posho hizo zisingetolewa kwa watumishi wanaotumia muda wa asubuhi kuzungukia miradi yao na kupiga porojo, halafu ikifika saa 9:30 ndiyo wanaanza kuwajibika vile inavyopasa.

Huo ni wizi, tena wizi wa mchana kweupe ambao haufai hata kidogo kufumbiwa macho hasa katika utekelezaji wa bajeti hii ya mwaka 2010/11, ili iweze kuzaa matunda yale yanayotarajiwa.

Inawezekana kabisa viongozi wetu wanayo nia nzuri ya kuleta unafuu wa maisha kwa watanzania. Lakini bado wapo watendaji wachache, wanathamini zaidi nafsi zao, hivyo kuamua kwa makusudi kuvuruga nia nzuri ya viongozi wetu. Kwakuwa baadhi ya watendaji wa namna hiyo wanafahamika, basi hatua kali za kinidhamu zianze kuchukuliwa dhidi yao kuanzia Julai mwaka huu, ili wakumbuke kwamba wapo katika ofisi hizo kuwatumikia watanzania na si kutunisha matumbo yao.

Au pengine uanzishwe utaratibu wa kuwepo kwa masanduku maalum ya maoni, ambapo yatatumika kubainisha majina ya maofisa wanaozorotesha jitihada za serikali ya awamu ya nne katika kutekeleza ahadi zake.

Fikra Pevu itafurahi zaidi endapo mkazo huo utawekwa kwa kuanzia katika Halmashauri zilizopo nchini ili mapato yake yapande kufikia angalau asilimia 20 ya mapato yote ya ndani. Hakika inatia aibu kwa Halmashauri hizo kutarajiwa kukusanya jumla ya shilingi 172.582 bilioni sawa na asilimia 2.9 ya mapato ya ndani yanayokusanywa na Serikali Kuu katika mwaka wa fedha 2010/11.

Kama alivyosema Waziri wa Fedha katika hotuba yake, kiwango hicho ni kidogo ikilinganishwa na fursa zilizopo katika mazingira ya Serikali za Mitaa. Ni vema eneo hilo likatupiwa kurunzi ya aina yake, ili mapato yaweze kuimarika na kuboreka, hivyo kubadili mfumo wa maisha wa wananchi wanaoishi katika Halmashauri hizo.

Pamoja na upungufu unaojionyesha kwenye Halmashauri, bajeti ya 2010/11 iko poa, ni jukumu letu kuitekeleza na kuitafsiri kwa vitendo.

*Mwandishi wa safu hii anapatikana kwa simu: 0713 077588