Wednesday, June 8, 2011

Uhuru wa vyombo vya habari, bila habari

Na Samson Kamalamo

KILA Mei 3 ya kila mwaka, ulimwengu huwa unaadhimisha Siku ya Uhuru wa vyombo vya habari duniani.

Mwaka huu kaulimbiu ya siku hiyo inasema: “Ukimya unaua demokrasia, lakini vyombo huru vya habari vinazungumza”.

Kimsingi ni kaulimbiu inayojaribu kuchochea vyombo vya habari kuzungumza zaidi na hasa masuala ya kijamii ambayo kwayo yameonekana kusahaulika.

Soma magazeti ya kila siku na kila wiki, sikiliza redio na kama haitoshi angalia matangazo ya vituo mbalimbali vya televisheni; vyote vimesheheni masuala ya siasa, mapigano na mauaji. Hivi ni kweli vyombo vya habari vipo katika kuangazia maeneo hayo tu?

Ni wazi kuna mahala vyombo vya habari vimepoteza mwelekeo na kujikuta vikishindwa kutimiza wajibu wake wa kuwapasha habari wananchi hasa zile zinazowahusu. Sitaki kuamini kuwa wasomaji wa magazeti na wasikilizaji wa redio wanavutiwa zaidi mambo ambayo yamekuwa yakiripotiwa na vyombo hivyo.

Ukweli ni kwamba hawapendi. Sisi wanahabari na mabwana zetu yaani wamiliki, ndiyo tunaoamua kipi tuwalishe wasomaji na wasikilizaji wetu. Hakika hatuwatendei haki hata kidogo.

Kwa upande wa Tanzania Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari uadhimishwa kwa namna nyingi, mojawapo ikiwa ya kuwatunikia Tuzo waandishi walioshinda katika nyanja mbalimbali za uandishi wa habari kwa mwaka mzima.

Hii inawezekana kuwa njia sahihi ya kuenzi siku hii, lakini pia bado kuna mapungufu makubwa katika tasnia hiyo ya habari nchini, kiasi cha Fikra Pevu kusema kuwa ni Siku ya uhuru wa vyombo vya habari, bila habari.

Fikra Pevu inaona ni siku ya uhuru wa vyombo vya habari, bila habari kutokana na ukweli kwamba, ziko habari nyingi ambazo zingepaswa kuandikwa, lakini haziandikwi, na kwamba waandishi wa habari wa Tanzania tunayo fursa ya kuandika mambo mengi ya msingi kuhusu nchi yetu lakini hatuandiki.

Huu ni uzembe unaostahili kupigiwa kelele na kila mwanataaluma na hata hao wanaodhamini mashindano ya wanahabari katika kuadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari.

Ingependeza kama kila mwaka kungewekwa agenda za msingi ambazo vyombo vyetu vya habari vingepaswa kuzijadili na kuzizungumzia kwa kina, halafu siku ya uhuru wa vyombo vya habari itumike kama sehemu ya kutathmini mafanikio yaliyofikiwa na hata kushindwa kufanikiwa.

Kwa mfano, ukifuatilia kwa ukaribu vyombo vyote vya habari vya Tanzania kwa miaka takriban mitatu mfululizo, vimekuwa vikiandika na kuripoti kuhusu ufisadi, si kwa kufanya uchunguzi, bali kwa kunukuu wanasiasa wakisema.

Hivi kama kweli ufisadi ni tatizo na watanzania wamechoshwa nao, jitihada gani za makusudi zimefanywa na vyombo vyetu vya habari katika kuhakikisha wanaotuhumiwa kwa ufisadi wanafikishwa katika vyombo vya sheria?

Hapa kuna mchezo wa kupoteza muda na kubadilisha mwelekeo wa fikra za watanzania, kuacha kufikiria mambo ya msingi na kuimbishwa ufisadi kila kukicha.

Kama kweli hatutumiki, basi leo hii mahakama zetu zingekuwa zimesheheni makumi kama si mamia ya kesi za ufisadi. Lakini hilo haliwezekani kwa kuwa vyombo vingine vimekuwa haviandiki habari za kina, zenye ukweli na takwimu za uhakika na za kutosha kushawishi mamlaka husika kuchukua hatua stahiki.

Nadhani ufike wakati sasa, tuachane na kushabikia hoja zinazotolewa na vyama vya siasa zenye lengo la kucheza na akili za watanzania; na vyombo vyetu viandike na kujadili masuala ya msingi.

Kwa kuwa hakuna chama hata kimoja kilichoeleza namna ya kutibu ufisadi, basi agenda za vyombo vya habari nchini zingepaswa kuangazia bei za vyakula, bei za mafuta ya petroli na namna ya kujikwamua na suala zima la mfumuko wa bei. Hayo ndiyo mambo ya msingi kwa watanzania, mambo ambayo hata siku moja hayahubiriwi na vyama tunavyovishabikia.

Siku ya uhuru wa vyombo vya habari kwa Tanzania ingepaswa kuadhimishwa kwa vyombo vya habari kutoa ushuhuda, ni kwa jinsi gani vimeweza kubadili maisha ya watanzania kwa mwaka uliotangualia na vitakavyoendelea kuboresha katika mwaka unaokuja na si kushabikia mitazamo ya kisiasa kama ilivyo sasa.

Wasalaam…

No comments:

Post a Comment