Sunday, October 24, 2010

NEC teknolojia izae matunda mema

JUMA lililopita Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitangaza kwamba matokeo ya kura za urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu yatakuwa ya kwanza kutolewa kabla ya matokeo ya ubunge na udiwani.

Kwetu watanzania hii ni faraja kubwa ikizingatiwa kwamba katika miaka iliyopita, matokeo yalichukua siku tano hadi kumi kutokana na mfumo wa ukusanyaji taarifa za matokeo ulivyokuwa, pamoja na jiografia ya nchi yetu.

Mwaka huu NEC imeamua kutumia teknolojia ya kisasa ya mawasiliano ambapo haichukui muda mrefu kwa matokeo ya kura za aina yoyote kuweza kuwekwa bayana kwa taasisi na jamii husika.

Haya naweza kusema ni mapinduzi, kwakuwa yatatuwezesha watanzania kumfahamu kiongozi mpya wa Tanzania katika kipindi kifupi baada ya watanzania kutumia haki yao ya msingi ya kumchagua Rais wao.

Ni dhahiri kuwa wapiga kura 19,686,608 waliojiandikisha kwa ajili ya kupiga kura Oktoba 31 mwaka huu, watakuwa na fursa nzuri ya kutambua matokeo ya maamuzi yao, pasipo kuwepo kwa uwezekano wa namna yoyote ile ya matokeo hayo kuchakachuliwa.

Fikra Pevu inaipongeza NEC kwa utaratibu huo mpya, kwakuwa umekuja wakati muafaka na inaamini kuwa utaondoa fikra za kuwepo kwa mazingira ya kura za rais kuchezewa na kutolewa matokeo yasiyo haki.

Ni kwa mantiki hii, vyama vya siasa nchini vinapaswa kujiweka tayari kupokea matokeo yoyote yatakayotolewa na NEC, siku moja baada ya watanzania kupiga kura.

Hatutarajii kwa vyovyote vile baada ya matokeo hayo ya urais kutangazwa tena kwa kushirikisha mawakala wa vyama katika vituo vyote vya kupigia kura, kutajitokeza madai ya kutokukubalina na matokeo yatakayotangazwa.

Ni vema kupitia uchaguzi huu wa nne wa demokrasia ya vyama vingi, wanasiasa na hasa wagombea, wakajifunza namna ya kukubali matokeo hata kama yatakuwa kinyume cha matarajio yao.

Kukubali matokeo, ni dalili za kukomaa kisiasa na hakuna sababu kwa wanasiasa wa Tanzania kuendelea kuwa wachanga ilhali mfumo wa siasa za Tanzania unaendelea kukua na kuimarika kila siku.

Kwakuwa NEC imeamua kutumia mfumo mpya wa kuwezesha kupatikana kwa matokeo kwa muda mfupi zaidi, ni wazi kuwa mfumo huo utazaa matunda mema na utakuwa chachu ya mabadiliko na maendeleo ya kidemokrasia nchini Tanzania.

Kama ambavyo teknolojia ya mawasiliano ilivyoweza kufanya kazi vema nchini Kenya mwaka 2007, ndivyo ambavyo tunaamini itatumika kutoa matokeo mema katika uchaguzi mkuu wa Tanzania mwaka huu.

Kwa utaratibu huu, tunaamini watanzania watakuwa na fursa ya kukwenda sanjari na mabadiliko ya kiteknolojia ambayo siku zote yanaaminika kutoa matokeo sahihi endapo hapatakuwepo na wajanja wachache watakaoamua kucheza matokeo hayo kwa maslahi yao binafsi.

Fikra Pevu inaamini kuwa hapatakuwepo na uchezeaji wa namna yoyote wa matokeo ya uchaguzi wa mwaka huu, ili kupunguza uwezekano wa kuwepo au kujitokeza kwa malalamiko ya aina yoyote ile. Kama upo uwezekano wa kuepuka malalamiko, basi nguvu za ziada zitumike kuondosha malalamiko ya aina hiyo.

Rai ya safu hii ni kwamba NEC itumie hiyo teknolojia mpya katika kuharakisha kupatikana kwa matokeo, izae matunda mema na si machungu.

Tuonane Juma lijalo.

No comments:

Post a Comment