MOJA ya mambo yanayonivutia sana katika siasa za Tanzania, ni kule kutaka kuziendesha kinyume na wenzetu wanavyo kwenda.
Inawezeka hiyo ikawa sababu ya Taifa hili kushindwa kusonga mbele na hata kurudi nyuma hadi leo. Tutasongaje mbele kama tunaweza kuwa na viongozi wanaofikiria kwenda kinyume na wenzao wanavyokwenda?
Ukisikiliza ahadi nyingi zinazotolewa majukwaani hivi sasa kama sehemu ya kuvutia wapiga kura, wanadi sera na ilani za vyama wamekuwa na ahadi kemkem.
Sikatai majukwaa hayo ya kisiasa kutumia kutoa ahadi hizo, kwa kuwa chaguzi zote zile duniani iwe Afrika, Ulaya na hata Marekani, hushehenezwa na ahadi za kila aina ili mradi kumvutia mpiga kura.
Ni kupitia ahadi hizo, ndipo wapiga kura wa Tanzania, Oktoba 31 mwaka huu, watatumia fursa yao ya kuchagua zile ahadi wanazoamini kuwa zitatekelezeka kutokana na uimara na ubora wake, na si vinginevyo.
Pamoja na kuwa ahadi ni sehemu ya kampeni, naweza kusema kwamba si kila ahadi inaweza kutekelezeka na si kila ahadi inaendana na hali halisi ya mazingira, siasa na uchumi wetu Tanzania kama taifa na maslahi ya nchi wahisani wa Tanzania, kama wadau wa demokrasia nchini.
Kweli tunatakiwa kutoa ahadi, lakini si ahadi zinazokwenda kinyume na taratibu zinazoongoza na kutawala dunia. Hatuishi katika kisiwa, hivyo hatupaswi kuwa na mitazamo na mienendo tofauti na pande nyingine za dunia.
Hata huko kwenye mataifa yaliyoendelea kama Marekani, Uingereza, Japan, Ujerumani, China, India na hata hapa katika nchi za Afrika zilizoko mbele kiuchumi kuliko sisi, huduma za afya na elimu hazitolewi bure kwa kila mmoja. Sasa hawa ndugu zetu wanaokuja na ahadi za kutoa huduma hizo bure, nguvu na ubavu wa kusema hivyo wanautoa wapi? Hapa ndipo hoja ya Mrisho Mpoto ya kumpa mbu kazi ya kutibu malaria inapokuwa na mashiko.
Kama hilo halitoshi, mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF Maalim Seif Sharif Hamad wiki iliyopita naye akaja na mpya ya kuturudisha nyuma, nayo si nyingine isipokuwa hoja ya serikali tatu.
Hivi ni kweli watanzania wanataka serikali tatu au ni mbinu ya kuwalaghai wapiga kura? Tunazungumziaje serikali tatu leo wakati dunia nzima inazungumzia kuungana? Tunapokuwa na serikali tatu tunaimarisha muungano au tunaudumaza?
Nafikiri ahadi za namna hii ni za alinacha na hazipaswi kupewa uzito hata kidogo katika jamii yenye fikra endelevu kama ya Tanzania. Ni kwa mkakati huo huo wa kudai serikali tatu, rafiki yangu Mchungaji Christopher Mtikila mara zote amejikuta akishindwa kisiasa kwa hoja yake ya serikali ya Tanganyika. Ndiyo anayohaki ya kuipigania, lakini si wakati huu.
Natambua CUF ni chama makini pengine kuliko vyama vyote vya upinzani vilivyopo, nisingependa hoja hii itumike kuwaangusha katika safari yenu ya kisiasa visiwani Zanzibar na hata Bara. Natoa rai hiyo kwa sababu natambua wenzenu wataitumia katika kuwapigilia msumari.
Katika uchaguzi huu, hoja ya serikali tatu haina mashiko hata kidogo, badili upepo Seif kabla haujakubadilikia.
Tukutane juma lijalo panapo majaliwa.
No comments:
Post a Comment