KATIKA moja ya habari za gazeti hili, kunazungumziwa namna Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilivyojizatiti kuhakikisha kinapata ushindi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Katika suala la uchaguzi kama ilivyo katika mpambano wa mpira wa miguu, huwa kuna kufa au kupona katika kusaka ushindi.
Zipo baadhi ya timu uenda mbali zaidi na kufikia hatua ya kutumia Kamati za Ufundi ili mradi wahakikishiwe kupata ushindi dhidi ya wapinzani wao.
Sidhani kama Kamati za Ufundi zinatumika pia katika vyama vya siasa hasa kwenye harakati za kusaka ushindi! Kama zinatumika, basi wanasiasa wetu ndiyo wenye nafasi kubwa ya kutujuza namna wanavyotumia kamati hizo kujinyakulia ushindi.
Katika siasa za kimaendeleo ambazo naamini Tanzania tunazifuata, kinachokipa chama fulani ushindi ni aina ya mgombea aliyesimamishwa, sera za chama husika na Ilani ya uchaguzi wa chama hicho.
Pale chama kinapochagua mgombea ama asiyeuzika au asiye na mvuto, ni dhahiri kuwa chaka hicho kitakuwa na asilimia kubwa ya kupoteza ushindi. Lakini pia uzoefu unaonyesha kuwa katika Tanzania yetu, bado suala la kufahamika kwa chama limekuwa mtaji mkubwa wa chama husika kupata ushindi.
Kwa mantiki hiyo ni kwamba, kama chama chako hakifahamiki, hakina mchango wowote unaonekana kwa wananchi, hata ufanye kitu gani, kamwe hautapata ushindi, utakuwa tu unauza maneno.
Ni kwa hoja hizo hapo juu, ndipo narudi kwenye mada ya leo ya rafiki zangu CHADEMA ya kutaka kuchukua hatua za kujitangazia ushindi kabla Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haijatangaza.
Ni kweli CHADEMA kama chaka kinacho kila sababu ya kujua na kufahamu idadi gani ya kura za ndiyo na hapana zimepigwa katika kituo fulani na chama gani kimepata kura nyingi, halikadhalika chama kipi kimepata kura kidogo, lakini si kujitangazia ushindi.
Rafiki zangu hawa wakifikia hatua ya kujitangazia ushindi, ni wazi watakuwa wamekiuka taratibu na kanuni za uchaguzi za nchi hii, na kwa maana nyingine wataufanya uchaguzi usiwe huru na haki.
Nisingependa CHADEMA waingie kwenye doa la kuvuruga uchaguzi na nchi kwa ujumla. Hata kama wanadhani kuwa huwa wanaibiwa kura zao, ni vema wakakusanya takwimu na kuziwasilisha zinakohusika, ikibidi kura za eneo fulani zirudiwa kuhesabiwa au uchaguzi wa jimbo husika ufanyike upya, lakini si kujitangazia ushindi.
Kama CHADEMA wataamua kujitangazia ushindi katika kila jimbo wanalodhani kuwa wataibuka na ushindi, itakuwaje CUF, CCM, TLP, NCCR-Mageuzi na vyama vingine navyo vikiamua kufanya hivyo?
Ningependa na ningeshauri rafiki zangu CHADEMA watumie busara kidogo katika kuendesha na kufanikisha uchaguzi huru na haki nchini, badala ya kuwa chanzo cha vurugu na mfarakano.
Ndiyo, wanaweza kabisa kuwa chanzo cha vurugu na mfarakano kama ilivyotokea nchi jirani ya Kenya, endapo watapinga matokeo yatakayotangazwa na NEC kwa kigezo kwamba matokeo hayo hayawiani na waliyonayo.
Ni vema CHADEMA wakasubiri matokeo ya kura zitakazopigwa Oktoba 31 mwaka huu yakatangazwa na chombo husika, badala ya wao kujivisha majukumu ya NEC na kujitangazia matokeo.
Tutakuwa na hakika gani kwamba matokeo yatakayotangazwa na CHADEMA yatakuwa ya haki ilhali naye ni mshindani katika kusaka madaraka ya kisiasa ya nchi hii?
Kama kweli wanajiamini na kujihakikishia kuibuka na ushindi, wana sababu gani ya kuharakisha kutangaza matokeo? Hapa kuna jambo na huenda si dogo kama ambavyo wengi wetu tunadhania.
Napenda kumalizia kwa kutoa rai kwa ndugu zangu wa CHADEMA pamoja na jukumu kubwa mlilonalo la kulinda kura zenu, ni vema misingi, taratibu, kanuni na maadili ya uchaguzi huru na haki ikafuatwa, ili kuepuka vurugu, ghasia na mifarakano isiyokuwa na maana.
Kushindwa leo hakuna maana ya kushindwa daima, huenda bado hujafikia kiwango cha kukubalika na kuaminika. Matokeo yoyote ya uchaguzi yanapaswa yachukuliwe kama fursa ya kufanya vema katika uchaguzi mkuu utakaofuata, ndivyo demokrasia inavyosema. Hii ni kwa vyama vyote na si kwa CHADEMA tu.
Tuwasiliane wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment